MAHAFALI MTANDAO YA WANAFUNZI 667 WA AKU KUTOKA MABARA MATATU YAFANA

 


Mahafali ya kwanza ya kimtandao kwa wanafunzi 667 kutoka mabara matatu ya Afrika, Asia na Ulaya waliokuwa wanasoma Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) yamefanyika hii leo na kushuhudiwa na mamilioni ya watu.

Akiwahutubia wanafunzi hao kwa njia ya mtandao, mwanzilishi na mkuu wa chuo hicho Mtukufu Aga Khan amesema anajivunia mchango unaotolewa na wahitimu wa chuo hicho kwenye kada mbalimbali ikiwemo kupambana na janga la Covid-19 huku akipongeza jitihada na ujasiri wa idara, watumishi na wanafunzi.

Mtukufu Aga Khan amesema anajivunia wahitimu kutoka Tanzania, Pakistan, Kenya, Uganda na Uingereza walioamua kuchagua “njia ya kutoa huduma kwa utu”.

“Chuo kikuu kimeonesha tofauti muhimu – kushauri serikali za mataifa, kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya wa sekta ya umma, kufanya kazi na walimu na shule mbalimbali, kukuza uelewa na ufahamu wa mambo kupitia vyombo vya habari na uandishi na kufanya kila linalowezekana kutibu wagonjwa na kuokoa maisha ya watu”. Ameongeza Mtukufu Aga Khan

Naye mwenyekiti mwenza na mdhamini wa taasisi ya Bill & Melinda, Melinda French Gates amekipongeza chou hicho kwa uongozi wake katika kuboresha afya na kuwainua wanawake.

Mbali ya hayo pia Melinda Gates ameonesha Imani yake kwa wahitimu wa mwaka huu.

“Chuo Kikuu cha Aga Khan sio tu ni rasilimali kubwa ulimwenguni, ni nguvu ya kimapinduzi kwa afya ya jamii na afya za wanawake. Tunajivunia kuwa na ushirikiano wa miaka mingi na AKU”. Ameongeza Melinda Gates

Mashirika ya Bill & Melinda Gates Foundation na Aga Khan Development Network ikiwemo chou kikuu cha AKU wanashirikiana kwenye kuboresha afya, kukuza maendeleo ya kiuchumi na kutengeneza fursa kwa wanawake na wasichana katika nchi za Afrika Mashariki na nchi za Afghanistan, Pakistan na India.

Hadi sasa taasisi hiyo imeshatoa takribani dola milioni 90 (Zaidi ya Tshs bilioni 200) za kusaidia kwenye utafiti na miradi mingine kwenye Chuo kikuu cha AKU ikiwemo afya ya uzazi na watoto, magonjwa ya kuambukiza, utapiamlo na Covid-19.














No comments

anonymous